Kocha wa Crystal Palace, Frank de Boer ametimuliwa baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa siku 77 pekee na sasa nafasi yake itachukuliwa na kocha wa zamani wa England, Roy Hodgson.
De Boer, 47, kocha wa zamani wa Ajax, alichukua kazi hiyo ya mwanzoni mwa msimu huu, akichukua nafasi ya Sam Allardyce aliyeondoka baada ya kuinusuru timu na janga la kushuka daraja.
Crystal Palace imepoteza mechi zote nne za mwanzo huku ikishindwa kudumbukiza wavuni hata bao moja, hatua ambayo haijawahi kufikiwa tangu mwaka 1924.
Frank de Boer anakuwa kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi kwenye kibarua chake na inakuwa ni mara ya pili kukutana na rekodi hiyo mbaya.
Mwaka 2016 alitimuliwa Inter Milan baada ya kuikochi kwa siku 83 tu.