MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini, amesema kitendo cha klabu hiyo kumuidhinisha Pep Guardiola kuwa kocha mpya kwa msimu ujao ni sawa na yeye kuonekana mjinga.
Kocha huyo alisema uamuzi huo wa haraka wa kumtangaza kuwa kocha mpya wa Manchester City msimu ujao, ulimuumiza kiasi cha kujiona yeye ni mjinga.
Meneja huyo raia wa Chile anamaliza mkataba wake wa miaka mitatu wa kubakia Etihad wakati mkurugenzi wa klabu hiyo, Txiki Begiristain, akiwa ameshakamilisha taratibu zote kwa Guardiola kuwa kocha mpya msimu ujao
Kocha huyo ambaye anaonekana kutoridhika kuondoka katika klabu hiyo, alisema, pamoja na ukweli kwamba Guardiola ni kocha mzuri ambaye amepata mafanikio kadhaa, lakini hata na yeye amefanya kazi nzuri.
Hata hivyo, alisema kilichomsikitisha ni kwamba hivi sasa amekuwa hana uhusiano mzuri na bodi ya klabu hiyo na kwamba imemtelekeza kiasi cha kuamini kuwa wanamuona mjinga.
Alisema, hafikirii kuwa amefanya kazi mbaya katika klabu hiyo, lakini ni jukumu la klabu hiyo kufanya tathmini ya kazi yake na kumuona kocha mpya anapaswa kuendeleza kile ambacho klabu inahitaji.
“Sifikiri kuwa wanataka kumleta Guardiola kwa kutarajia makubwa, ila ameletwa kwa sababu Begiristain aliwahi kufanya kazi naye katika klabu ya Barcelona.”