MKONGWE na nguli wa filamu za kitamaduni, Fadhili Msisiri, ameendelea kuthibitisha kuwa, roho mbaya na imani za kishirikina, ni kati ya vikwazo vya maendeleo katika sana ya filamu hapa Bongo.
Akiongea na Saluti5, Msisiri alisema kuwa, wasanii wengi wa filamu hapa nchini wamekuwa ni watu wasiopenda maendeleo ya mwingine, huku baadhi yao wakiwa tayari hata kwenda kwa waganga ili kuwarudisha nyuma wenzi wao kimaendeleo.
“Utakuta msanii anaandaa filamu na kuacha kumpa shavu yule mwenye uwezo kwa hofu ya kumpandisha chati zaidi na kumfunika, ambapo badala yake humtafuta msanii wa kawaida na kumchezesha, bila kujali kuwa anaishusha kiwango muvi yake,” alisema Msoisiri.
Msisiri alisema kuwa, umefika wakati sasa kwa wasanii wote kuwa kitu kimoja na kupenda kushirikiana, ili kuipandisha juu zaidi sanaa ya filamu, badala ya kukazania kubaniana pamoja na kujawa na imani za kishirikina.