Simulizi moja ya zamani inasema vipofu wawili katika kijiji fulani walibahatika kukuta tembo amekufa, wakatumia fursa ile ‘kutalii’ kwenye mwili wa mnyama yule mkubwa zaidi duniani.
Basi vipofu wale wakamzunguka tembo yule na kujaribu kuupapasa mwili wake ili kubaini ukubwa wake na walipomaliza kila mmoja akawa na jibu lake.
Kipofu wa kwanza akasema kumbe tembo ni mkubwa kama gari, huyu alibahatika kuushika mwili wote wa tembo, lakini yule wa pili ambaye aliishia kushika sikio tu, akasema kumbe tembo ni mdogo kama ungo.
Ubishi uliozuka hapo ulikuwa mkubwa sana, hata wapita njia waliojaribu kuwasaidia kwa kuwaambia kuwa aliyesema tembo ni mkubwa kama gari hakuwa mbali na ukweli, yule aliyeshika sikio bado alisisitiza kuwa mnyama yule ni mdogo kama ungo.
Naam hata katika muziki na filamu zetu za Kibongo, wako watu kibao wenye fikra kama hizo kuwa tembo ni mdogo kama ungo. Hata utumie njia gani watakubishia kwa nguvu zao zote.
Sanaa ni kama mchezo wa ‘draft’, anayecheza haoni mchezo kwa makini kama mtazamaji, hii inaashiria kuwa kama wewe ni msanii au promota basi ni muhimu kuchukua maoni ya watu wa nje maana wao wana jicho kali kuliko wewe uliye ndani ya ‘game’.
Katika kundi lenye watu wabishi na wasiokubali ushauri kirahisi basi bongo movie na muziki wa dansi wanaongoza. Huku ndiko kwenye wajuaji ambao neno “kukosolewa” ni msamiati mgumu kwao.
Ni katika bongo movie ndio unapoweza kukutana na ‘cover’ (jalada) la sinema ambayo muhisika kavaa nguo ambazo hutaziona hata kwa sekunde moja ndani ya filamu yenyewe. Muhusika anaweza kuonekana kwenye ‘cover’ amesuka rasta, lakini ndani ya sinema ukamkuta kanyoa upara. Sasa kosoa hilo uone moto wake.
Ni katika bongo movie ndiko utakutana muhusika mwenye jina kubwa kwenye ‘cover’ akiwa kawekwa kama muhisika mkuu (staring) lakini ndani ya sinema yenye part 1 na 2, utamuona kwenye ‘scene’ moja tena labda part 1 peke yake.
Ni katika bongo movie ndipo utashuhudia jambazi anaua mtu, kisha mtoto mdogo aliyeshuhia baba yake akiuwawa anakuja kulipa kisasi akiwa mtu mzima huku jambazi yuko na umri uleule, staili ileile ya nywele na mavazi, gari lile lile tena halijachakaa hata kidogo. Ukihoji utaambiwa huna ujualo.
Ni katika dansi tu ndipo unapoweza kukutana na tangazo (poster) la bendi kubwa ambalo limepambwa hadi na wasanii marehemu waliotangulia mbele ya haki. Ukikosoa unaonekana msaliti.
Ni katika dansi ndipo unapoweza kukutana pia na poster ya bendi ambayo ndani yake ina wanamuziki waliohama bendi zaidi ya mwaka mmoja. Ukihoji unaambiwa mtengenezaji wa poster hajui wasanii wa dansi, lakini cha ajabu wahusika wa show au bendi wanakuwa wa kwanza ‘kupost’ mitandaoni posters hizo zenye makosa ya aibu. Lakini huku pia ndipo unaweza kukuta hata jina la bendi linakosewa kwenye tangazo lakini likavumiliwa.
Ni katika muziki wa dansi ndipo mwenye bendi anaweza kukataa milioni moja ya promota lakini akakubali laki sita ya mwenye bar ili akapige show za kiingilio kinywaji. Sijui mmliki huyu ana tofauti gani na kipofu aliyesema tembo ni mdogo kama ungo.
Wakati wanamuziki wa kizazi kipya hawaoni choyo kusifia ujuzi wa wasanii wa dansi, mambo huwa ni kinyume pale unapotaka kujua watu wa dansi wanajifunza nini kwa watu wa bongofleva. Jibu utakalopewa ni jepesi tu …wale si wanamuziki ni wababaishaji, mwanamuziki wa kweli lazima ajue kupiga muziki wa ‘live’.
Inachukuliwa dosari moja tu na kufanywa kama fimbo, huku mambo mengine kibao mazuri na yenye mafanikio kwa wasanii wa kizazi kipya yakifumbiwa macho. Hii inawezekana kwa wasanii wa dansi tu. Ni muhimu kutambua kuwa muda wako una kikomo, jiwekee mazingira ya kukumbukwa kwa mambo ya msingi.