Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye mambo sasa yako hadharani. Khalid Chokoraa amerejea rasmi Twanga Pepeta.
Habari za uhakika zilizopenyezwa Saluti5 zinasema Chokoraa ameamua kurejea nyumbani na kwamba tayari ameshaaga viongozi wenzake wa Mapacha Watatu.
Msanii huyo aliyekuwa mmoja wa wakurugenzi wa Mapacha Watatu anafanya idadi ya wanamuziki waliowahi kuwa wakurugenzi kufikia watatu ndani ya Twanga Pepeta.
Wanamuziki wengine waliowahi kuwa wakurugenzi wa bendi ni Ally Chocky (Extra Bongo) na Kalala Jr (Mapacha Watatu).
Chokoraa aliibuliwa na Extra Bongo mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kuhamia Twanga Pepeta mwaka 2005 na kudumu nayo hadi mwaka 2010 alipoanzisha Mapacha Watatu yeye na Kalala Jr pamoja na Jose Mara, hiyo ikiwa ni baada ya mpango wao wa Mapacha Wanne kuingia kwi kwi mwishoni mwa mwaka 2009.
Kwa Takriban wiki tatu, Saluti5 ilikuwa ikiandika mara kwa mara juu ya mpango wa Twanga Pepeta kumrejesha kundini aidha Chokoraa au Chaz Baba, lakini sasa jibu liko hadharani. Ni Chokoraa.
Afisa mmoja wa Aset inayomiliki Twanga Pepeta ambaye hakutaka kutajwa jina, ameithibitishia Saluti5 kuwa Chokoraa anarejea Twanga na atatambulishwa kwa onyesho kubwa litakalofanyika Jumamosi ya wiki ijayo Juni 4 ndani ya Mango Garden Kinondoni.
Kiongozi huyo wa Aset amesema Chokoraa anatua Twanga Pepeta na rap mpya itakayojulikana kama “Tumbua Jipu”.
Naye afisa mmoja wa Mapacha Watatu ameiambia Saluti5 kuwa ni kweli Chokoraa anaondoka lakini wana matumaini kuwa angalau atamalizia maonyesho ya wiki hii kabla ya kwenda kutambulishwa rasmi Twanfa Pepeta.