Sasa tunahesabu masaa tu kabla ya bendi ya African Stars “Twanga Pepeta” kuzindua albamu yake ya 13 ijulikanayo kwa jina la “Usiyaogope Maisha” mkoani ndani ya ukumbi wa Villa Park jijini Mwanza Jumamosi hii.
Akizungumza na Saluti5 mkurugenzi wa ASET inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka alisema kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika na wanamuziki wake wapo kwenye ari ya hali ya juu.
Mbali ya wimbo wa “Usiyaogope Maisha” uliotungwa na Ally Chocky, nyimbo nyingine zinazounda albamu hiyo ni “Ndoa” (Luizer Mbutu), “Uso Chini”, (Chocky), “X-Michepuko” (Msafiri Diouf), “Mapenzi Yanaumiza” (Haji Ramadhani) na “Ganda la Muwa” uliotungwa na Saleh Kupaza ambaye kwa sasa anaitumikia Ivory Band.
Asha alisema kuwa wamekwisha rekodi nyimbo zote na mauzo ya CD 1000 ya kwanza, yatatumika kuchangia ununuzi wa madawati mkoani Mwanza. Alisema kila CD itauzwa Sh3, 000 ambapo Sh 1,000 watatumia kununua madawati.
Bendi ya Super Kamanyola yenye maskani ya kudumu Villa Park ndiyo itakayoisindikiza Twanga Pepeta katika uzinduzi huo.
Albamu za nyuma ya bendi hiyo ni Kisa Cha Mpemba, Jirani, Fainali Uzeeni, Chuki Binfasi, Ukubwa Jiwe, Mtu Pesa, Safari 2005, Password, Mtaa wa Kwanza, Mwana Dar es Salaam, Dunia Daraja na Nyumbani ni Nyumbani.