
MAROUANE FELLAINI alikuwa ndani ya Stadio Olimpico akiitazama Roma ikicheza na Napoli siku ya Jumatatu, huku wakala wake, Luciano D'Onofrio akisema staa huyo kuhamia Serie A ni jambo linalowezekana.
Wakati D'Onofrio akitoa kauli hiyo, gazeti la michezo la Italia, Gazzetta dello Sport, limeripoti kuwa Roma wana shauku ya kutaka kumsajili kiungo huyo wa Manchester United.
Kuhusu Fellaini kuonekana Italia, D’Onofrio aliiambia Tuttomercatoweb kuwa pengine alikuwa kwenye mapumziko.
"Kwa sasa sina habari nyingine. Hadi sasa sina mawasiliano na Roma kwa ajili yake,” alisema D’Onofrio na alipoulizwa kama mteja wake anaweza kuhamia huko akasema; “Ndiyo, upo uwezekano wa kuifikiria Roma.”
Fellaini alisajiliwa Manchester United na David Moyes akitokea Everton miaka mitatu iliyopita, ambapo kwa msimu huu amecheza mechi 32 katika mashindano yote zikiwamo 17 za Premier League.