STRAIKA Robert Lewndowski ameweka bayana dhamira ya kutaka kuachana na Bundesliga ifikapo mwishoni mwa msimu wa mwaka 2019.
Kauli hii inakuja siku chache tu baada ya kuwepo kwa tarifa kuwa bosi wake wa Bayern Munich, Jose “Pep” Guardiola tayari ametangaza kutua katika kikosi cha Manchester City ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo, kuna tetesi kuwa Lewndowski ana asilimia kubwa ya kumfuata bosi wake (Guardiola) katika klabu ya Manchester City na kwamba taarifa za hivi sasa kutangaza kuondoka Bayern ni mwanzo tu wa kukamilisha dili hilo.
City tayari imeweka bayana mkakati wa kutaka kumsainisha straika huyo ifikapo mwanzoni mwa msimu wa mwaka 2016 kwa dau la pauni 45 mil.
Pep ambaye ni kocha wa mabingwa hao wa Ujerumani, ameshakamilisha mazungumzo na uongozi wa juu wa Manchester City na kukubaliana kila kitu kinachohusiana na maslahi ya kandarasi yake hiyo mpya.
Wakala wa Lewndowski, Cezary Kucharski, amenukuliwa akikiri kuwa tayari ametaarifiwa juu ya utayari wa kuondoka kwa straika huyo aliyetua Bayern akitokea Dortimund.
Kucharski alibainisha pia kuwa mchezaji huyo tayari ameonyesha nia ya kuhama kutoka Bundesliga na huenda akatua England au Hispania.
Taarifa za uwezekano wa kuhama kwa mpachika nyavu huyo zinakuja kufuatia gazeti la Telegraph kuanika tetesi za hivi karibuni za kutakiwa na klabu za Barcelona na Manchester United.
Akinukuliwa zaidi, wakala huyo alisema; “Ninafikiri inawezekana kuwa ni ofa ya hali ya juu kwake kuhama kutoka Bayern lakini haitakuwa chini ya euro 50 mil.”
“Robert ni kati ya wachezaji walio na thamani kubwa kwa sasa ambao wako sokoni kwa ajili ya msimu huu wa usajili wa majira ya kiangazi.”
“Kila timu inamtaka Robert kwa gharama inayofanana na hadhi aliyonayo, kwasababu ana uwezo mkubwa wa kufunga magoli hasa katika mazingira tofauti.”
“Thamani yake hupanda kadri miaka inavyokwenda, kwavile yuko katika kiwango cha juu kwani ana wastani mzuri wa kupachika mabao nyavuni.”
“Ukiwana mchezaji wa hadhi ya Robert unaweza ukajivunia kuwa na kikosi cha ushindi na ninaamini anaweza kwenda katika Ligi kama ya England ama ya Hispania lakini kwa kukubali ofa wanayoitaka Bayern Munich,” alisisitiza wakala huyo.