HII inaweza kuwa taarifa murua masikioni mwa mashabiki wa muziki wa mduara, hususan wale waliokipokea kwa mikono miwili kibao ‘Moyo Kama Macho’ cha mfalme wa Kibao Kata, Jumaa Kivurande ‘Kivurande Junior’.
Taarifa yenyewe ni kuwa, video ya wimbo huo ambao kwa sasa unaonekana kuwa habari ya mujini baada ya kukubalika zaidi kila kona ya Tanzania, imekamilika na wakati wowote inaweza kumwagika mtaani.
Akiongea na Saluti5, Jumaa Kivurande amesema kuwa, video hiyo ambayo picha zake zimechukuliwa maeneo ya Dar es Salaam, Tanga na Mombasa, Kenya na ambayo iko katika ubora wa hali ya juu, imepangwa kuachiwa mwishoni mwa mwezi huu.