BEKI wa kati wa Simba, Abdi Banda amekiri kwamba alifanya makosa katika mechi dhidi ya Kagera Sugar kwa kumtandika ngumi mchezaji wa timu hiyo, Geogre Kavila.
Baada ya Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kumfungia mchezaji huyo mechi mbili, ameibuka na kusema kwamba alikosea lakini akaahidi hatarudi tena kosa hilo.
Baada ya tukio hilo Banda alipelekwa kwenye Kamati ya nidhamu na kuadhibiwa kukosa mechi mbili za Ligi Kuu lakini kwa kuwa alisimamishwa kucheza na amekosa mechi dhidi ya Mbao FC na Toto African ni kama adhabu yake imekamilika.
“Namshukuru Mungu suala langu limeisha, nimekoma na kuna kitu nimejifunza maana nilijiona mkosefu kwa kujadiliwa na watu wengi," amesema Banda.
"Sitarudia tena kitendo kama kile licha ya mchezo wa soka kuwa na majaribu mengi ambayo yanaweza kukufanya uchukue uamuzi wowote ule, nimejifunza na kuanzia leo mimi ni mtu mwema,” amesema.
Amesema, kukosa kwake mechi mbili hakutamuathiri kwa kuwa yeye ni mchezaji mkubwa na anachokiangalia hivi sasa ni kuisaidia timu yake iweze kutwaaa ubingwa.
Shirikisho la soka nchi limesema kwamba pamoja na kuliomba, pia Banda alishamuomba radhi Kavila na hivyo adhabu yake haikuwa kali sana kutokana na uungwana wake.