Manchester United wamelazimika kwenda hadi dakika 30 za ziada (Extra time) ili kufuzu hatua ya nusu fainaili ya Europa League.
Hatua hiyo iliwasili baada ya United kulazimishwa sare ya 1-1 na Anderlecht ya Ubelgiji katika dakika 90 za kawaida, matokeo yaliyolandana na yale ya mchezo wao wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita.
Wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafford, United kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza, walitangulia kupata bao dakika ya 10 mfungaji akiwa yule yule Henrik Mkhitaryan.
Anderlecht wakasawazisha dakika ya 32 mfungaji akiwa Sofiane Hanni, matokeo yakabaki hivyo hadi dakika 90 za kawaida zilipomalizika.
Marcus Rashford akawa shujaa kwa Manchester United baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi dakika ya 107.
United ilipata pigo dakika ya 22 baada ya kumpoteza beki wake Marcos Rojo aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daley Blind.