TIMU ya soka ya Madini FC ya Arusha imesema iko tayari kuvaana na wekundu wa Msimbazi Simba SC Jumapili hii katika Kombe la Shirikisho la soka Tanzania (TFF).
Madini watakuwa wenyeji wa Simba katika mchezo war obo fainali wa Kombe la ASFC uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mjini Arusha wakihitaji ushindi kusonga mbele.
Kocha wa Madini FC, Abdallah Juma amesema kuwa kikosi chake kipo kamili kuwavaa Simba siku ya Jumapili na hakuna majeruhi yeyote katika kikosi chake.
Amesema kwamba kikosi chake kipo kambini kujiandaa na mchezo huo na amewataka mashabiki wa soka wa mkoani Arusha na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ya Madini.
Akiongea kwa tahadhari kuelekea mchezo huo, kocha Juma amesema anaamini kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, watashinda pambano hilo kwani katika mchezo wa soka chochote kinaweza kutokea licha ya Simba kuwa timu kubwa na inayoheshimika nchini na barani Afrika.
Kwa upande wao mashabiki wa soka mkoani Arusha wameonekana kuusubiri mchezo huo kwa hamu kubwa kutokana na mkoa huo kukosa timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa takriban miaka mitatu sasa.
Madini iko Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara na kufikia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayorushwa mojakwamoja na kituo cha Televisheni cha Azam, ilizitupa nje JKT Oljoro ya Arusha, Panone ya Kilimanjaro na JKT Ruvu ya Pwani.