KIPINDI cha Choice Bambataa cha kituo cha radio cha Choice FM cha jijini Dar es Salaam, kinakuja na mkakati mzuri wa kuunyanyua muziki wa dansi.
Choice Bambataa kimesema moja ya hatua zao za kuusukuma mbele muziki wa dansi, ni kusaidia kuwaingiza studio wanamuziki wa dansi na kurekodi nyimbo zao bure na kisha kufanyiwa promosheni ya hali ya juu kupitia kipindi hicho kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa.
Akiongea na Saluti5 mmoja wa watangazaji wa kipindi hicho cha Choice Bambataa, Irine Gabriel (pichani juu), alisema hawaangalii ukubwa wa jina la mwanamuziki, bali watakachoangalia ni uwezo na ubora wa kazi za msanii kulingana na soko la sasa.
“Lengo la kipindi chetu katika mpango huu, ni kuwasaidia wanamuziki wa dansi ambao wana kazi nzuri lakini hawana uwezo wa kuingia kwenye studio za kisasa na kurekodi nyimbo zao,” anaeleza Irine.
“Tutagharamia kuwaingiza studio na kuhakikisha wanaibuka na kazi zenye kiwango cha hali ya juu,” aliongeza mtangazaji huyo wa Choice Bambataa.