STRAIKA wa Matajiri wa Stanford Bridge, Pedro amesisitiza azma yake ya kuendelea kubaki Chelsea, licha ya kuweko na taarifa kuwa anajipanga kwa ajili ya kurejea Hispania.
Pedro alijiunga na ‘The Blues’ akitokea Barcelona kwa dau la pauni 21.4 mil lakini taarifa za sasa hivi zinasema ana mpango wa kuondoka katika Ligi Kuu ya England.
Klabu ya Atletico Madrid imekuwa ikitajwa katika orodha ya timu zinazomwania straika huyo mwenye umri wa miaka 28.
Tetesi hizo zinatokana na hatua ya kocha Jose Mourinho kutemwa na matajiri hao ambapo bosi huyo Mreno ndie aliyemleta Pedro darajani.
Pedro anasema: “Nina furaha nikiwa hapa. Nayazungumza haya kwa imani ya moyoni, ninajivunia kuwa katika klabu kubwa.”
“Nina furaha na mashabiki wa timu hii ingawa ni kweli kuwa hali ya mambo hapa si shwari hata kidogo lakini kwa pamoja tunaweza tukaipandisha timu kutoka hapa.”