Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka wamiliki wa bar, kumbi za starehe, viongozi wa bendi na wanamuziki watii sheria ya kumaliza muda wa maonyesho yao hadi pale sheria hiyo itakapobadilishwa.
Makonda aliyasema hayo katika mkutano wake na wanamuziki, wamiliki wa bendi, wamiliki wa kumbi za starehe na wadau wa muziki uliofanyika Alhamisi mchana ndani ya ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni.
Washika dau hao wa muziki waliitisha mkutano huo na kumwalika Mkuu huyo wa Mkoa ili kumlilia kutokana na agizo lake alilolitoa hivi karibuni la kutaka bar na kumbi za starehe zisizo na vidhibiti sauti (sound proof) kutopiga muziki baada ya saa 6 usiku.
Makonda alisema: “Maombi yangu kwangu kwenu nyinyi ni mawili na naomba mnielewe.
“Ombi langu kwanza naomba mnielewe kuwa sina uwezo wa kupindisha sheria hata niwe nawapenda vipi.
“La pili nataka kikao hiki kizae matunda, kilishe mambo mawili – ya kwanza ni kutii sheria na pili ni kuzaa matunda ya kubadili sheria.
Makonda akaitaka kamati ya muda ya wanamuziki na wamiliki wa bar na kumbi za starehe iandae mapendekezo ya kubadili sheria hiyo, mapendekezo ambayo yatakuwa na hoja zenye mashiko na ushawishi wa kutosha uliojaa hoja za msingi.
Mkuu huyo wa mkoa akaahidi kuwa atayapeleka mapendekezo hayo kwa waziri husika na kwamba anaamini ndani ya muda usiozidi wiki mbili sheria hiyo itakuwa imefanyiwa marekebisho kwa mkoa wake wa Dar es Salaam.
“Dar es Salaam ni mji wa kibiashara, sasa hivi tunaandaa utaratibu utakaoruhusu maduka ya kariakoo na posta kufunguliwa hadi saa 4 za usiku, kwahiyo hata hili la bar na kumbi za starehe linazungumzika kwa Dar es Salaam,” alisema Makonda.
“Tunajua kuna ajira kubwa sana kwenye sekta ya muziki wa bendi, bar na kumbi za starehe, lakini pia kuna pato kubwa ambalo serikali inavuna kupitia upande huo, hivyo zitakapokuja hoja za msingi nina imani sheria hii inaweza ikabadilishwa,” aliongeza Mheshimiwa Makonda.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa alitahadharisha kuwa ni lazima muziki uangaliwe unapigwa kwenye mazingira gani.
“Kama bar au ukumbi upo jirani na shule, hospitali, msikiti au kanisa na athari ya muziki unaotoka huko ni kero kwa maeneo hayo niliyoyataja, basi ukumbi huo utapoteza sifa ya kupiga muziki,” alitahadharisha Makonda.
Mheshimiwa Makonda pia alisema grocery na bar zinazopiga muziki barazani, hazitavumiliwa.
Kamati ya muda ya wanamuziki na wamiliki wa bar na kumbi za starehe inaundwa na watu kadhaa wakiwemo Mzee Yussuf, Asha Baraka, Juma Mbizo, Siza Mazongela, Khadija Kopa,Ismail Rashid “Sumagar” na Juma Jerry “JJ”.
Mmoja wa wanakamati ya wadau wa muziki Ismail Sumaragar (kulia) akimkaribisha akimpokea Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa koa akiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya wadau wa muziki

Siza Mazongela katibu wa muda wa kamati ya wadau akifungua rasmi mkutano
Mwenyekiti wa muda wa kamati ya wadau Juma Mbizo akitoa hutuba fupi iliyoandaliwa na wadau
Sehemu wadau wa muziki waliojitikeza Vijana Social Hall kuongea na Mkuu wa Mkoa
Watu walifika kwa wingi bila kujali mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam
Sehemu nyingine ya wadau
Mkuu wa Mkoa akisisitiza jambo