DIEGO MARADONA ametoa wito kwa Bodi ya Klabu ya Napoli kuupiga bei mtambo wao wa mabao, Gonzalo Higuain (pichani), na kumsajili straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane kuziba nafasi yake.
Napoli iliwauza mastaa wake huko nyuma kwa bei nono, hasa Ezequiel Lavezzi aliyekwenda Paris Saint-Germain, na Maradona anahisi kuwa klabu itaweza kujenga kikosi kizuri zaidi kwa kumtoa Higuain – raia mwenzake wa Argentina.
"Namjua rais (wa Napoli) na nadhani atamuuza Higuain. Tayari tuliona kilichotokea kwa Ezequiel Lavezzi na jinsi Napoli ilivyotumia fedha kwa ufanisi," alisema kocha huyo wa zamani wa Argentina.
"Unaweza kujenga timu nzuri kwa fedha ulizotengeneza kwa mauzo makubwa. Unahitaji kuona sura mpya uwanjani na hii inaweza kutokea kama watamuuza Higuain kwa bei kubwa."
Higuain, straika wa zamani wa Real Madrid, amekuwa na msimu wa mafanikio, akifunga mabao 30 katika mechi 32 za Serie A.
"Si rahisi kuziba nafasi ya Higuain, lakini kama itakuwa juu yangu, ningalimchagua Harry Kane kutoka Tottenham. Sijui atagharimu kiasi gani, lakini ningalipenda kumsajili bila kusita," alisema.
Kane amekuwa na msimu bora akifunga mabao 24 katika mechi 35 za Premier Leagua msimu huu, na tayari anatolewa macho na klabu kubwa barani Ulaya, ikiwamo Manchester United, huku Spurs ikiamini nyongeza ya mkataba ghali zaidi itatosha kumbakisha White Hart Lane.