
CRISTIANO RONALDO alikosa mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Champions League wakati Real Madrid ilipotoka 0-0 na Manchester City Uwanja wa Etihad Jumanne usiku, kutokana kuwa na majeraha madogo, lakini amedai kuwa kama ingekuwa fainali angeliingia dimbani kucheza.
Ingawa alitarajiwa kucheza mchezo huo baada ya kuumia paja wikiendi iliyopita, straika huyo Mreno alifeli mtihani wa kuthibitisha uzima wake na hakuwa na nafasi hata katika benchi, nafasi yake akipewa Lucas Vasquez.
Straika huyo akiongeza na Antena 3 wakati wa mapumziko Etihad alisema: "Ni busara; Nasubiri mchezo ujao. Kama ingalikuwa fainali, ningalicheza."
Naye straika mstaafu wa Real Madrid, Emilio Butragueno Santos, aliiambia Bein Sports kwamba bado Ronaldo alikuwa na maumivu hivyo ilikuwa bora kwake kutocheza.