Kwa mara nyingine tena, Double M Plus itamimina uhondo wa burudani leo usiku ndani ya Equator Grill ambapo bosi wa bendi hiyo Mwinyuma Muumin anatarajiwa kufunika tena sana kwa masauti yake matamu.
Ijumaa iliyopita Double M Plus ilitimua vumbi ndani ya ukumbi huo kwenye onyesho la kufungua pazia ya ratiba yao ya kutumbiza Equator Grill kila Ijumaa.
Double M Plus ikadhihirisha kuwa ina utajiri wa program ya nyimbo pendwa (hit songs) kuanzia zile za Mchinga Sound, Tam Tam na Double M Sound ambako kote huko Muumin alishiriki kuzalisha kazi nyingi zilizotesa ndani na nje ya Bongo.
Nyimbo kama “Kiu ya Mapenzi”, “Tunda”, “Mgumba”, “Kilio Cha Yatima”, “Kisiki Cha Mpingo” na nyingine nyingi zilinguruma Equator Grill na kusisimua mashabiki waliofika kwenye ukumbi huo ulioko maeneo ya Mtoni, Temeke jijini Dar es Salaam.
Ni uhondo kama huo, ndio unaotarajiwa kujirudia tena leo usiku ndani ya Equator Grill.